You are here:-, What's New-HOTUBA YA MHE. DKT. PHILIP MPANGO, (MB.), WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO, KWENYE HAFLA YA KUZINDUA UPYA JUMUIYA YA WACHUMI

HOTUBA YA MHE. DKT. PHILIP MPANGO, (MB.), WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO, KWENYE HAFLA YA KUZINDUA UPYA JUMUIYA YA WACHUMI

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA WIZARA YA FEDHA NA MIPANGO HOTUBA YA MHE. DKT. PHILIP MPANGO, (MB.), WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO, KWENYE HAFLA YA KUZINDUA UPYA JUMUIYA YA WACHUMI TANZANIA (THE ECONOMIC SOCIETY OF TANZANIA – EST) UKUMBI WA BENKI KUU YA TANZANIA (BOT), DAR ES SALAAM, 24 FEBRUARI, 2018 2 HOTUBA YA MHE. DKT. PHILIP MPANGO, (MB.), WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO, KWENYE HAFLA YA KUZINDUA UPYA JUMUIYA YA WACHUMI TANZANIA (THE ECONOMIC SOCIETY OF TANZANIA – EST) Bw. Geoffrey Mwambe, Mkurugenzi Mkuu wa TIC na Mwenyekiti wa Kamati Iliyoongoza Maandalizi ya Mkutano Huu; Prof. Florens Luoga, Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania na Mwenyeji Wetu; Wageni Mashuhuri na Maafisa Waandamizi wa Serikali Mliopo; Viongozi wa Sekta Binafsi; Wachumi Wenzangu na Marafiki; Waandishi wa Habari; Mabibi na Mabwana. UTANGULIZI: Napenda nianze hotuba yangu kwa kutoa shukrani zangu za dhati kwa Kamati ya Maandalizi ya mkutano huu kwa kunialika na kunipa heshima kubwa ya upendeleo ya kuwa Mgeni Rasmi kwenye uzinduzi wa Jumuiya ya Wachumi Tanzania (The Economic Society of Tanzania).

Ninafahamu kwamba wapo Watanzania wenzetu ambao ni magwiji wa uchumi au fani nyingine na wanastahili zaidi kupewa heshima hii kuliko mimi. Hivyo, nilipokea mwaliko huu kwa unyenyekevu, lakini na wasiwasi pia! Wasiwasi wangu ulitokana na kuwa waandaji wa hafla hii hawakunidokeza kuhusu aina (calibre) ya waalikwa wa mkutano huu na matarajio yao, ili kuniwezesha kuandaa hotuba stahiki ya ufunguzi. Lakini kwa upande mwingine, ninawashukuru waandaji maana kwa kufanya hivyo wameniachia uhuru wa kusema kile ninachoamini kitasaidia kuchokoza mjadala utakaozaa jumuiya imara na endelevu ya Wachumi Tanzania (a strong and sustainable professional association of Economists in Tanzania). Aidha, nitatumia jukwaa hili kusema machache kuhusu ajenda ya Serikali ya awamu ya tano, chini ya Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, yenye lengo la kufanya mabadiliko makubwa ya kiuchumi nchini. Nitaeleza kidogo kuhusu Utekelezaji na changamoto. Lengo langu ni kuanza kuweka mezani ajenda za tafiti na mijadala kwa ajili ya siku za usoni, chini ya jukwaa la EST mpya, itakayosaidia kuipeleka Tanzania kwenye ngazi ya juu zaidi kimaendeleo.

UONGOZI NA AJENDA YA JUMUIYA YA WACHUMI TANZANIA: Wachumi Wenzangu, Nchi kuwa na jumuiya au chama hai cha Wachumi na chenye nguvu ni muhimu sana. Naomba mniruhusu nitoe sababu tatu kusisitiza umuhimu wa kufufua EST. Kwanza tasnia 3 ya uchumi ina nafasi ya pekee sana katika kazi ya kujenga nchi kijamii, kiuchumi na hata kisiasa. Aidha, mtakubaliana nami kuwa katika maeneo mengi, wachumi tunategemewa tuwe viongozi. Bila shaka waumini wenzangu wa John Maynard Keynes mliopo katika ukumbi huu mtakumbuka maneno yake. Nanukuu: “The ideas of economists and political philosophers, both when they are right and when they are wrong, are more powerful than is commonly understood. Practical men who believe themselves to be quite exempt from any intellectual influence, are usually the slaves of some defunct economist.” Tafsiri isiyo rasmi ni kuwa: Mawazo ya wachumi na wanafalsafa wa siasa, yawe sahihi au si sahihi, yana nguvu kuliko inavyoeleweka kwa wengi. Watu wanaojiamini kwamba wako huru na ushawishi wa wanataaluma, kiuhalisia watu hao ni watumwa wa mchumi fulani marehemu! Mabibi na Mabwana, Sababu ya pili inatokana na ukweli kwamba siku za usoni hazifahamiki mia kwa mia na sisi wachumi hatuna anasa ya kufanya majaribio na maisha ya watu katika maabara (laboratory experiments) kama wenzetu upande wa sayansi asilia (natural sciences). Mathalani, endapo utafanya majaribio na misingi ya uchumi-jumla (macro-economic fundamentals) kiuhalisia bila shaka moto utawaka! kwa maana ya mfumuko wa bei kupanda, thamani ya sarafu kuanguka, uzalishaji kushuka, wananchi kukosa huduma za msingi, vijana kukosa ajira n.k.

Athari kama hizi nazo huchochea maandamano mitaani ambayo yanapelekea kuanguka kwa serikali nyingi! Ili kuepuka kufanya makosa makubwa kupita kiasi, mbadala wa maabara kwa Wachumi ni uwepo wa jukwaa la mijadala ya kukosoana na kubadilishana mawazo kuhusu sera na mwenendo wa uchumi wa Taifa, kuchangamkia fursa zinazojitokeza na namna ya kukabiliana na dhoruba za kiuchumi mbele yetu (head winds). Wageni Waalikwa na Wachumi Wenzangu, Sababu yangu ya tatu ni haja ya kuondokana na madhara makubwa yanayotokana na kutokuwepo jumuiya hai ya kusimamia kazi za Wachumi hapa nchini. Baadhi ya athari ni zifuatazo: (i) Baadhi ya watu kudai wana shahada za uchumi lakini kiuhalisia ni mbumbumbu wa uchumi; (ii) kutungwa kwa sera au kufanyika kwa maamuzi yasiyoendana na taaluma ya uchumi kunakopelekea kuumiza wananchi masikini kutokana na uwepo wa wachumi feki ambao wanapewa nafasi za kazi serikalini, vyuoni na hata katika sekta binafsi; (iii) Kukosekana kwa udhibiti wa vyeti, stashahada na shahada hususan vinavyopatikana au kutengenezwa kwenye mitandao ya kompyuta; (iv) kuharibika kwa sifa za wachumi wazuri wa Tanzania na vyuo vyetu vinavyofundisha wachumi machoni pa sekta binafsi ya ndani na nje kwa Imani kwamba samaki mmoja akioza basi wameoza wote; na (v) Serikali kukosa fursa pana ya kupata njia mbadala 4 (options) za kuharakisha maendeleo ya kiuchumi na kijamii nchini. Nionavyo mimi, madhara haya yanayotokana na kutokuwepo kwa jumuiya ya Wachumi iliyo hai na imara hapa nchini, ni kubwa mno. Hivyo, naomba sana, zamu hii tufanye tofauti kurekebisha hali hii na natumaini itakuwa ni kwa mara ya mwisho (once and for all). Wachumi wenzangu, Baadhi yenu mtakumbuka kuwa The Economic Society of Tanzania (EST) ilisajiliwa kwa mara ya kwanza tarehe 15 Novemba 1966 (miaka 52 imepita) na ikapewa hati ya usajili Namba S.A. 5198 tarehe 26 Juni 2013 na Wizara ya Mambo ya Ndani, chini ya Sheria ya Societies Act, Cap.337 [R.E. 2002]. Malengo makuu ya kuanzisha EST yalikuwa ni pamoja na kuilinda tasnia ya wachumi nchini, kuwaunganisha wachumi, kusimamia weledi wa wachumi, kuhamasisha na kuimarisha utafiti na uchambuzi wa taarifa, kupitia sera na mipango mbalimbali ya maendeleo ya Serikali kwa ujumla na kisekta na kuimarisha mahusiano na taasisi zingine. Hata hivyo, imepitia miaka takriban 20, kuanzia mwaka 1998 hadi hivi sasa, ambapo Jumuiya yetu imekuwa mfu au haionekani kuwepo au kutoa mchango wowote kwa nchi yetu kama ambavyo ilikusudiwa!! Wachumi Wenzangu, Kwa kweli haipendezi kuona kwamba wakati tasnia nyingine mfano Uhandisi, Jiolojia, Sheria, Uhasibu, n.k. wana vyama vyao vya kitaaluma vilivyoshamiri, inaonekana sisi Wachumi tu ndiyo tumeshindwa kukaa pamoja na kuendesha jumuiya yetu! Inavyoonekana, kikwazo kikubwa kimekuwa ni udhaifu wa kiuongozi na kitendaji. Nimejaribu pia kupekua kwenye intaneti na nimeona nchi kama Kenya, Afrika Kusini, Nigeria, Singapore, Philippines, Australia, Uingereza, China na kadhalika, wanazo jumuiya hai za wachumi.

Kulikoni sisi Wachumi wa Tanzania kushindwa kujifunza kutoka nchi nyingine namna ya kuendesha jumuiya yetu? Tena ukitugawa sisi Wachumi katika michepuo yetu mbalimbali unaona mapungufu mengi zaidi yanayotokana na ombwe hili la kutokuwepo kwa Jumuiya ya Wachumi. Wakati mwingine huwa najiuliza: Je, ukuaji duni wa sekta ya kilimo na biashara husika (agribusiness) una uhusiano wowote na udhaifu wa usimamizi na ukosefu wa mijadala chanya ya wachumi katika tasnia ndogo ya uchumi wa kilimo? Kadhalika: Je, kukosekana kwa mijadala na tafiti za wachumi wa viwanda, public finance, kunachangia kudumaza ukuaji wa sekta za viwanda, upanuzi wa wigo wa kodi au kuhakikisha matumizi adili ya fedha za umma? Vivyo hivyo, ninajiuliza kuhusu changamoto za kidemografia, mazingira, na miundo ya kiuchumi (economic institutions) hapa nchini. Labda magwiji mliofika leo mtanisaidia kupata majibu. Wachumi Wenzangu, Mabibi na Mabwana, Kwa maoni yangu, hitaji la kuwa na jumuiya hai na yenye nguvu ya Wachumi, halina mjadala. Mimi naamini kwa dhati kabisa kwamba dhana na malengo ya kuasisi EST mwaka 1966 yana maana zaidi (more relevant) nyakati hizi za kidigitali, utandawazi, mabadiliko ya haraka ya teknolojia, ubunifu na uvumbuzi, nafasi muhimu na ya kipekee 5 ya sekta binafsi katika kujenga uchumi wa Taifa na pia ushindani mkali wa kibiashara ikilinganishwa na ilivyokuwa katika miaka hiyo ya sitini. Nikiazima msemo wa Dkt. Shika, “itapendeza” kuwa na EST iliyosisimka (vibrant)! Na ili hili litimie tutahitaji kuchagua viongozi wenye uwezo, dhamira ya dhati na elimumwendo (committed and dynamic) tena wanaoheshimika kitaaluma (not mediocre) ambao watawajibika kikamilifu na hawatatuangusha. Hatua inayofuata baada ya mkutano huu iwe ni vitendo (walk the talk). Mabibi na Mabwana, Napenda tena kuwapongeza wote walioona umuhimu wa kuzindua upya Jumuiya ya Wachumi Tanzania. Ni vizuri tuwatambue na kuwapongeza taasisi chache na watu binafsi ambao wamekuwa wanakerwa na ombwe hili na kuamua kuchukua hatua kuifufua The Economic Society of Tanzania (EST). Taasisi hizo ni Idara ya Uchumi Chuo Kikuu cha Dar-es-Salaaam, Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Tanzania Investment Centre (TIC), NSSF, TTCL, TIB, na TTCRA. Aidha, niruhusuni niwataje kwa majina waliobuni wazo hili la kufufua EST na kutukutanisha hapa leo. Watu hao ni Geoffrey Mwambe, Gedion Mchau, Dkt. Aikael Jehovaness, Frederick Shirima, Dkt. Joel Silas, Gloria Mbiha, Vidah Malle, Dkt. Innocent Pantaleo, Aristides Mbwasi, Moses Mwizarubi, Dkt. Thereza Mtenga, Dkt. Lihoya Antoni, Nicholas Shombe na bila kumsahau Prof. Samuel Wangwe. Aidha, ninawashukuru pia ninyi nyote mliofika. Wingi wenu hapa leo tena siku ya mapumziko ya mwisho wa wiki unadhihirisha kuwa tupo Wachumi wengi tunaotamani uwepo wa EST hai na endelevu. Pia nawashukuru wale ambao wametuandalia mada za kusisimua majadiliano yetu leo na pia wafadhili wa mkutano huu ikiwa ni pamoja na Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania na Uongozi mzima wa Benki Kuu ya Tanzania ambao wameturuhusu kutumia ukumbi huu mzuri wa mikutano. MAGEUZI YA KIUCHUMI CHINI YA UTAWALA WA MAGUFULI NA MWELEKEO BAADA YA 2025: Wachumi Wenzangu na Marafiki, Tunakutana leo ikiwa ni takriban miaka miwili tangu Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliposhika hatamu za uongozi wa Taifa letu la Tanzania.

Vipaumbele vya Serikali ya awamu ya tano vimebainishwa katika Hotuba ya Rais ya kuzindua Bunge aliyoitoa tarehe 20 Novemba 2015. Vipaumbele hivyo kwa upande wa uchumi ni: (i) Kutatua malalamiko ya wananchi hususan rushwa katika utoaji huduma, uzembe, uvivu na urasimu, pamoja na kudhibiti uvujaji wa mapato, ufisadi, wizi, ubadhirifu na matumizi mabaya ya fedha za umma, na kuondoa kodi na tozo za kero; (ii) Kuimarisha msingi imara wa kiuchumi uliojengwa katika awamu zilizotangulia; (iii) Kuimarisha upatikanaji wa huduma muhimu za jamii (maji, afya, elimu); (iv) Kuimarisha miundombinu ya usafiri na usafirishaji (reli, barabara, usafiri wa majini na anga) na umeme; (v) Kuendeleza kilimo mifugo na uvuvi na hususan kuongeza thamani, kuongeza tija na uzalishaji kwa 6 kushughulikia uhaba wa zana na pembejeo, uhaba wa masoko ya uhakika, maghala, na huduma za ugani; (vi) Kuhakikisha madini na rasilimali zetu zinatumika kwa manufaa ya Taifa; Kuweka mkazo mkubwa katika ujenzi wa viwanda; na (viii) Kupambana na tatizo la umasikini na ajira. Mabibi na Mabwana, Ni dhahiri kuwa mafanikio ya kuridhisha yamepatikana katika kipindi hiki kifupi cha miaka miwili katika maeneo yote niliyoyataja. Tanzania sasa ni kinara wa vita dhidi ya rushwa na kupiga vita uzembe na uvivu katika utumishi wa umma ikiwa ni pamoja na kuwaondoa watumishi hewa na wale wenye vyeti feki kutoka kwenye utumishi wa umma. Hatua kali zimechukuliwa kupambana na ufisadi na kudhibiti matumizi mabaya ya fedha za umma na biashara ya madawa ya kulevya. Uchumi wa Taifa kwa ujumla umeendelea kuwa thabiti. Tanzania imebakia kuwa miongoni mwa nchi 10 za bara la Afrika ambazo uchumi wake unakua kwa kasi zaidi (Kati ya Julai na hadi Septemba 2017 Pato la Taifa lilikua kwa wastani wa 6.8%. Aidha Tanzania ni moja ya nchi ambazo zinaongoza kwa upande wa upatikanaji wa huduma jumuishi za kifedha (financial inclusion) na hapa napenda kuwashukuru wenzetu wa BoT kwa kulisimamia hilo. Sarafu ya Tanzania imebaki kuwa imara na mfumuko wa bei umedhibitiwa na kubakia katika wigo wa tarakimu moja. Katika kipindi cha Julai mpaka Desemba 2017 mfumuko wa bei ulikuwa wa wastani wa 4.8%. Serikali imeongeza nguvu katika ukusanyaji wa mapato na kupambana na ukwepaji kodi. Matokeo yake ni kuwa mapato yameongezeka kutoka wastani wa shilingi 850 bilioni kwa mwezi wakati wa awamu ya nne kufikia wastani wa shilingi trilioni 1.2 kwa mwezi hivi sasa.

Aidha kupitia bajeti ya serikali kodi nyingi na tozo za kero zimefutwa. Akiba ya fedha za kigeni imeongezeka kufikia US$5,911.2 milioni (Novemba 2017) kiasi hiki kinatosha kuagiza bidhaa na huduma kutoka nje kwa zaidi ya miezi 5. Mabibi na Mabwana, Katika kipindi hiki cha miaka miwili Serikali imeanza kujenga miradi mikubwa ya miundombinu ikiwemo reli mpya ya kati kwa kiwango cha standard gauge, na miradi mkubwa wa umeme Kinyerezi (kwa kutumia gesi asilia) na mto Rufiji eneo la Stigler’s gorge. Aidha, Serikali imechukua hatua za kufufua shirika la ndege ATCL kwa kununua ndege na pia meli mpya kuimarisha usafiri wa majini. Mafanikio mengine ni kujenga viwanja vya ndege na barabara za lami zikiwemo barabara za juu Dar es Salaam, na kuongeza upatikanaji wa dawa na vifaa tiba. Pia Serikali imetekeleza azma yake ya muda mrefu ya kuhamishia makao makuu Dodoma ili pamoja na faida nyinginezo kuweza kujenga kitovu kingine cha ukuaji uchumi nchini (growth pole) katikati ya nchi. Sambamba na jitihada hizi za Serikali, kumekuwa na mwitikio mzuri wa sekta binafsi kuwekeza katika uanzishwaji wa viwanda vidogo na vya kati (vifaa vya ujenzi, uunganishaji wa pikipiki na matrekta, madawa, vifaa vya kufundishia, nyama, vinywaji na juisi, uzalishaji wa mafuta ya mbegu) hasa katika mikoa ya Pwani na kanda ya Ziwa. 7 Mabibi na Mabwana, Ni wazi kuwa zimekuwapo changamoto pia. Licha ya kuwa na kasi kubwa ya ukuaji wa Pato la Taifa, ukuaji huu bado hauonekani sana katika maisha ya wananchi walio wengi kiuhalisia.

Baadhi ya changamoto ni pamoja na kasi ndogo ya ukuaji wa sekta ya kilimo (chini ya wastani wa 3%) ambayo ndiyo tegemeo la Wananchi wengi. Katika nusu ya kwanza ya 2017 sekta ya kilimo ilikua kwa 3.1%; Pia ukosefu wa ajira (10.3%) na kiwango cha umasikini nchini bado ni kikubwa. Inakadiriwa kuwa Watanzania takriban milioni 15 (28.2% ya idadi ya watu) wanaishi chini ya kiwango cha umasikini wa mahitaji ya msingi; Upatikanaji wa maji safi na salama na huduma za afya bado haukidhi. Baadhi ya madhara ya huduma hafifu za afya ni pamoja na vifo vingi vya watoto chini ya miaka mitano (67 kwa kila vizazi hai 1,000) na vifo vya mama wajawazito (556 kwa kila vizazi hai 100,000) na pia kuna umuhimu wa kuongeza ubora wa elimu. Vilevile Tanzania inakabiliwa na changamoto ya kasi kubwa ya ongezeko la idadi ya watu (2.7% kwa mwaka) na wastani wa watoto 5.2 kwa kila mwanamke (total fertility rate) na inakadiriwa kuwa idadi ya watu itafikia milioni 54.2 mwaka huu 2018. Sekta ya fedha imekumbwa na msukosuko ikiwemo kuongezeka kwa mikopo chechefu (hasa katika shughuli za biashara na kilimo) kufikia 12.5% (Septemba 2017) ikilinganishwa na ukomo wa 5% uliowekwa na Benki Kuu, pia riba za kukopa zimeendelea kuwa kubwa na ukuaji wa mikopo kwa sekta binafsi kuongezeka kwa kasi ndogo; Baadhi ya biashara zimedorora hususan zile ambazo awali zilizokuwa hazilipi kodi ipasavyo na zile zenye madeni makubwa. Wabia wengi wa maendeleo kutoka nje wamechoka kutoa misaada na kujiondoa kwenye misaada ya kibajeti; kupanda kwa gharama za mikopo katika mabenki na taasisi za fedha za kimataifa; uwepo wa hatari au dhoruba nyingi katika uchumi wa dunia kama vile wepesi wa bei ya mafuta kupanda au kuanguka kwa bei za bidhaa katika soko la dunia; na ulaghai unaotekelezwa na makampuni ya uwekezaji kupitia mikataba isiyo na tija kwetu. Aidha pamekuwepo upinzani dhidi ya baadhi ya hatua hizi za kijasiri (bold reform actions) hususan kutoka kwa watu wachache na masahibu wao waliokuwa wananufaika na mfumo wa zamani ambao ulikuwa hauna tija wala uendelevu. Wachumi Wenzangu, Niliona nieleze haya kwa sababu ninaamini kuwa ni vema Wachumi tuanze sasa kufikiri namna tutakavyo kusanya nguvu na maarifa ili kuongeza kasi ya kuibadilisha Tanzania yetu kuwa kitovu cha uchumi katika Afrika baada ya kipindi cha Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025 kumalizika, na mahali pa kuanzia ni kutambua wapi tulipo hivi sasa (where do we stand today).

Hivyo, pamoja na jitihada tunazofanya kuendeleza nchi yetu na kukabiliana na changamoto zilizo mbele yetu, ni lazima tuanze kuangalia mbele Zaidi. Ni vema tujiulize dunia itafanana namna gani miaka 25 au 50 ijayo na tunataka Tanzania iwe wapi katika dunia hiyo? Je, nguvu yetu kuu (motor) itakayotupeleka kuifikia Tanzania tunayoitamani sambamba na kuhimili dhoruba zitakazojitokeza mbele yetu ni nini? Tunahitaji maandalizi gani katika maeneo mbalimbali ya kimkakati ili fursa zisituponyoke? 8 Ni muhimu pia tujitambue kwamba mambo yamebadilika na kwamba katika dunia ya leo kwenda mbele hakuna mjomba! Ni namna gani tutatumia rasilimali zetu vizuri na kujenga moyo na ari ya kila Mtanzania kutumia uwezo na vipaji vyake kwa ajili ya kuijenga nchi yetu? Naomba niwajulishe kuwa kwa upande wa Serikali tayari tumeanza hatua za awali kujiandaa na kubuni dhima na dira ya maendeleo ya nchi yetu baada ya mwaka 2025. Hivyo, natoa wito kwa watakaochaguliwa kuwa viongozi wa EST mpya na Wachumi wenzangu nchini kote, kuanza kutafakari, kujipanga na hatimaye kuchangia kwa bidii na weledi katika mchakato huo muhimu sana kwa maendeleo ya mama Tanzania. HITIMISHO: Wachumi Wenzangu, Mabibi na Mabwana, Naomba nihitimishe kwa kueleza matarajio yangu. Matarajio yangu ni kuwa kuanzia leo Tanzania itakuwa na Jumuiya ya Wachumi (EST) yenye nguvu itakayojengwa juu ya misingi ya weledi na utaalam, elimu na ujuzi, bidii, uzalendo, uwazi na uwajibikaji (professionalism and meritocracy, knowledge and skills, diligence, nationalism, transparency and accountability).

Aidha, ningependa kuona Jumuiya ya Wachumi ambayo itajitanabaisha kwa kwa (i) umahiri wa kukuza utafiti wa kiuchumi, maendeleo ya nchi na mafunzo ya Wachumi kazini, (ii) Kuratibu jukwaa la mijadala kuhusu sera za kiuchumi na maendeleo ya Taifa letu la Tanzania kwa ujumla na katika Jumuiya ya Afrika Mashariki, (iii) Kuibua mawazo mbadala na yanayotekelezeka ya kuiweka Tanzania katika nafasi ya kuwa kitovu na nguvu kuubwa ya uchumi katika bara la Afrika; na (iv) Kuratibu mfumo wa mahusiano na Wachumi na vyama vingine vya Wachumi (networking) katika nchi za bara la Afrika na kwingineko na ikiwa pamoja na ushiriki wa Wachumi kutoka Tanzania katika majukwaa mbalimbali ya kiuchumi yenye maslahi kwa Taifa letu. Wachumi Wenzangu, Mwisho kabisa, napenda niwatambue na kuwapongeza sana Wachumi wazalendo ambao wameiweka nchi yetu ya Tanzania katika ramani ya dunia ya Wachumi mashuhuri. Wa kwanza ni marehemu Prof. Justinian F. Rweyemamu. Wa Pili ni Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete Rais Mstaafu wa awamu ya nne, na wa Tatu ni Prof. Benno J. Ndulu Gavana mstaafu wa Benki Kuu ya Tanzania.

Hawa kwa maoni yangu wanastahili tuzo na napendekeza EST mpya itafakari vigezo na namna bora ya kuwatambua na kuwaenzi Wachumi hawa weledi na vilevile kuwatambua Wachumi wengine wenye sifa kama hizo, na hata Wachumi chipukizi ili kuwatambua na kulea vipaji vyao. Wachumi Wenzangu, Wageni wetu, Mabibi na Mabwana, Kwa heshima na taadhima, naomba sasa nitamke rasmi kuwa The Economic Society of Tanzania (EST) imezinduliwa rasmi upya. 9 ASANTENI SANA KWA KUNISIKILIZA

By | 2019-05-29T16:18:06+03:00 February 24th, 2018|Categories: Uncategorized, What's New|0 Comments